Tovuti ya TACAIDS  inalenga  kusambaza taarifa muhimu za  VVU na UKIMWI kwa jamii, pamoja na kubadilishana uzoefu na wadau wanao tekeleza afua za UKIMWI nchini, ili kuboresha mapambano ya UKIMWI na kufikia malengo yetu ya kuwa na Tanzania isiyo na maambukizi ya VVU.

Nyote mnakaribishwa.

Dkt. Leonard L. Maboko
MKURUGENZI MTENDAJI

Unapaswa kuwashawishi vijana kuacha kujihusisha katika masuala ya ngono hadi wanapoweza kufanya maamuzi makini. Iwapo lazima washiriki ngono, basi lazima wafanye ngono salama. Lazima watumie kondomu kwa usalama, usahihi na mara kwa mara. Wakati mwingine, mtu anaweza akawa mwaminifu kwa mwenzi wake lakini anaweza akawa haitambui hali ya VVU ya mwenzi wake wa ngono. Hivyo, ni muhimu kuwashawishi wote wawili wakapime VVU.

 

Kuelewa hali ya VVU kunawarahisishia watu binafsi kufanya maamuzi mahususi ya kupunguza tabia na mienendo hatarishi na kuongeza njia salama za kujamiiana. Kwa mfano, mtu asiye na VVU anachukua hatua za makusudi za kuishi bila virusi, na mwenye VVU naye anachukua hatua thabiti za kuepuka kumwambukiza mwenzi wake, anaepuka kuwaambukiza wengine, anafuata unasihi, anapata matibabu na kupanga maisha yake ya baadaye.

 

Kwa bahati mbaya, Watanzania wengi hawaifahamu hali yao. Kwa kweli, ni watu 14 tu katika watu 100 ndio ambao wamekwishapata kupimwa VVU. Hii ni idadi ndogo sana. Hivyo, jitihada za uzuiaji zinapaswa kushughulikia umuhimu wa kwenda kupima kwa hiari na unasihi ili watu binafsi waweze kujilinda wao wenyewe, pamoja na wenzi wao wa ngono. Tunapaswa kutoa kipaumbele kwa vijana.

 

Takribani watu sitini katika watu mia moja walioambukizwa VVU ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 15-24? Watoto wetu wako katika hatari zaidi!

Watoto wetu walio wengi huanza ngono mapema. Hata kabla hawajafikia umri wa miaka 15! Unapaswa kufahamu kwamba wasichana wengi huacha shule baada ya miaka saba tu ya elimu. Na, hata hivyo, kadiri wanavyokaa shuleni muda mrefu zaidi, ndivyo ilivyo bora kwao. Watajifunza jinsi ya kusema kuwasiliana na wavulana na watu wazima wanaowakonyeza kwa kujiamini. Pia, watajifunza jinsi ya kusema HAPANA kwa sauti kubwa wanaporubuniwa kingono.

 

Kuna vipengele vingi ambavyo vina uwezekano wa kuchangia katika kufanya ngono mapema. 

Miongoni mwa vipengele hivyo ni:

  • Umaskini
  • Shinikizo rika kuanza uhusiano wa kingono
  • Ndoa za mapema zinazokubaliwa na utamaduni
  • Shughuli chache za burudani
  • Ukosefu wa stadi za majadiliano ya kuchelewesha kuanza kujamiiana
  • Kupatikana sehemu na muda ulioridhiwa kijamii kujishughulisha na ngono
  • Unyanyasaji wa kijinsia.
  • Mambo haya huwaweka vijana katika hatari kubwa sana, hususan kwa vile hawatumii kondomu!