Tovuti ya TACAIDS  inalenga  kusambaza taarifa muhimu za  VVU na UKIMWI kwa jamii, pamoja na kubadilishana uzoefu na wadau wanao tekeleza afua za UKIMWI nchini, ili kuboresha mapambano ya UKIMWI na kufikia malengo yetu ya kuwa na Tanzania isiyo na maambukizi ya VVU.

Nyote mnakaribishwa.

Dkt. Leonard L. Maboko
MKURUGENZI MTENDAJI

Matunzo na msaada nyumbani Masuala ya Kimkakati: 

Wagonjwa sugu wa UKIMWI mara nyingi wanatunzwa na familia na hasa na wanawake na watoto, ambao kwa kawaida hawana mafunzo ya kutosha yakiwemo ya msaada. Watoa mafunzo ya nyumbani huwasaidia na kuweka mwendeleo wa matunzo kwa kuunganisha vituo vya huduma za afya na jamii. Hata hivyo, mifumo ya rufaa ya pande mbili haitoshi kuwasaidia wagonjwa na familia zao ipasavyo katika kutambua na kuwaunganisha na watoa matunzo ya nyumbani na kupata matunzo ya vituo vya huduma za afya pale inapotakiwa.

Wakati mafunzo mengi ya watoa matunzo katika vituo vya huduma za afya na katika jamii yamefanywa katika miaka mitano iliyopita, uratibu na ushirikiano kati ya sekta ya umma na vyama vya kiraia bado ni mdogo. Ili kupanua huduma kwa WAVIU wengi na familia zao, ujengaji uwezo na ushirikiano lazima uimarishwe. Aidha kumekuwa na uzingativu mdogo uliotolewa kwa mahitaji ya mafunzo na msaada kwa watoa huduma za msingi katika jamii.

Kwa kuwahusisha zaidi na kwa wingi wasio wafanyakazi wa afya na WAVIU, upatikanaji wa huduma za matunzo nyumbani unaweza kuboreshwa zaidi. Hata hivyo, watoa huduma wote, lazima wapate mafunzo ya aina moja na kutumia mfumo mmoja wa utoaji taarifa na ufuatiliaji ili kuhakikisha ubora wa mafunzo katika ngazi ya jamii. Hata hivyo mafunzo yanayotumiwa lazima yawe yanafaa na kutumiwa na walengwa mahususi.

Huduma za matunzo nyumbani zimekuwa zikisaidiwa na AZISE mbalimbali na wabia wa maendeleo. Ili kueneza kwa haraka huduma kwa wilaya zote, jukumu la programu linahitaji kusimamiwa na Timu za Usimamizi wa Afya za Halmashauri na vivunge vya vifaa na dawa za matunzo ya nyumbani vya aina moja vitolewe katika ngazi hii, kwa kuzingatia kuwa wagonjwa hawa huenda wakaomba dawa kutoka vituo vya huduma za afya.

 

Lengo la Kimkakati: 

Kuongeza kuwepo na kupatikana kwa huduma bora za matunzo ya jamii na ya nyumbani. Mikakati:

1. Kuwafunza watoa matunzo wengi wanawake na wanaume wa vituo vya huduma za afya, na familia.

2. Kuimarisha uhusiano wa kiutendaji zikiwemo huduma za rufaa kati ya vituo vya huduma za afya na matunzo ya nyumbani.

3. Kuhimiza uraghibishi na shughuli za elimu ya umma katika jamii ili ziweze kukidhi ipasavyo mahitaji ya WAVIU na familia zao.

4. Kuhimiza ushiriki mkubwa wa WAVIU katika kupanga na kutekeleza huduma za matunzo nyumbani na misaada.

5. Kuhakikisha kuwa watoa huduma za matunzo wanaelewa haki stahiki kwa matunzo, matibabu na msaada kwa mujibu wa Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Matunzo za nyumbani.

 

Viashirio:

  1. Asilimia ya watu wazima wenye umri wa miaka 18 hadi 59 ambao wamekuwa wagonjwa sugu kwa miezi mitatu au zaidi katika kipindi cha miezi 12 iliyopita kutokana na VVU na UKIMWI, ambao kaya zao zimepata msaada wa msingi wa nje wa kuwatunza wagonjwa sugu watu wazima.
  2. Idadi ya asasi zinazotoa Huduma za Matunzo za Nyumbani.
  3. Idadi ya ziara za Watu za Huduma za Matunzo za Nyumbani.
  4. Idadi ya watoa Huduma za Matunzo za Nyumbani waliopata mafunzo kulingana na Mwongozo wa Taifa.