Tovuti ya TACAIDS  inalenga  kusambaza taarifa muhimu za  VVU na UKIMWI kwa jamii, pamoja na kubadilishana uzoefu na wadau wanao tekeleza afua za UKIMWI nchini, ili kuboresha mapambano ya UKIMWI na kufikia malengo yetu ya kuwa na Tanzania isiyo na maambukizi ya VVU.

Nyote mnakaribishwa.

Dkt. Leonard L. Maboko
MKURUGENZI MTENDAJI

Idadi ya vituo vya ushauri nasaha na upimaji (VCT) imeongezeka kiasi cha kuridhisha katika kipindi cha mwaka 2003 – 2007. Mwishoni mwa mwaka 2006 vilikuwepo vituo vya VCT 1,027 ukilinganisha na vituo 289 tu vilivyokuwepo mwaka 2003. Hivi ni pamoja na vituo vilivyoko katika vituo vya huduma za afya na vile vinavyojitegemea. Mgawanyo wa kijiografia wa vituo vya VCT bado hauna uwiano, vituo vingi viko mjini, japokuwa wilaya zote angalau zina vituo si chini ya vinne. Idadi ya wateja waliopata ushauri nasaha imeongezeka kufikia watu 680,520 katika mwaka 2006 kutoka karibu watu 140,000 waliopata ushauri nasaha mwaka 2003. Pamoja na usambazaji na upatikanaji wa huduma, bado uelewa wa ushauri nasaha na upimaji wa VVU ni mdogo sana nchini. Utafiti wa Kiashirio cha VVU/UKIMWI Tanzania (THIS) uliofanyika mwaka 2003/2004 ulionyesha kuwa kiasi cha 15% tu ya wanaume na wanawake wamewahi kupima VVU.

Wanaume na wanawake waishio mijini yawezekana kuwa wamewahi kupima VVU mara mbili au mara tatu zaidi ya wanaume na wanawake waishio vijijini. Moja ya sababu za kuwa na kiwango kidogo cha watu kujua afya zao ni pamoja na kuwepo na vituo vichache vya kutoa huduma hiyo, hasa vijijini, uelewa mdogo wa jamii kuhusu manufaa ya kujua hali yako ya VVU. Kuwepo na wataalamu wachache wenye uwezo wa kutoa ushauri nasaha na woga wa kunyanyapaliwa ni kati ya vikwazo vya kuongezeka kwa utumiaji wa huduma ya VCT, pia kukosekana kwa huduma na matunzo baada ya kupima. Kampeni ya Kitaifa ya hivi karibuni ya upimaji wa hiari wa VVU inalenga kuongeza idadi ya Watanzania wanaofahamu hali ya afya zao na kuchukua hatua za kujilinda wao wenyewe na kuwalinda watu wengine.