Tovuti ya TACAIDS  inalenga  kusambaza taarifa muhimu za  VVU na UKIMWI kwa jamii, pamoja na kubadilishana uzoefu na wadau wanao tekeleza afua za UKIMWI nchini, ili kuboresha mapambano ya UKIMWI na kufikia malengo yetu ya kuwa na Tanzania isiyo na maambukizi ya VVU.

Nyote mnakaribishwa.

Dkt. Leonard L. Maboko
MKURUGENZI MTENDAJI

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko Afrika Mashariki. Inashirikiana mipaka na Kenya na Uganda kwa upande wa kaskazini, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa upande wa magharibi, na Malawi, Zambia na Msumbiji kwa upande wa kusini. Bahari ya Hindi inafanya mpaka wa mashariki. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeundwa na Tanzania Bara na Zanzibar. Waraka huu unahusu Tanzania Bara tu. Tanzania Bara imegawanyika kiutawala katika mikoa 21 na wilaya 133, manispaa na halmashauri za miji. Tanzania inakadiriwa kuwa na watu takribani milioni 37 (hesabu ya 2005) ambapo asilimia 30 wanaishi mijini na asilimia 70 wanaishi vijijini. Idadi kubwa ya watu ipo kanda ya Ziwa, katika Ziwa Victoria kwa upande wa kaskazini na kuzunguka Dar es Salaam, kituo kikuu cha biashara katika mwambao, na kusini nyanda za juu katika Mkoa wa Mbeya. Maeneo makubwa ya nchi yana watu wachache waliotawanyika. Kiwango cha ongezeko la watu kinakadiriwa kuwa asilimia 2.8, na umri wa watu kuishi ni miaka 47 kwa wanaume na 49 kwa wanawake, zikiwemo athari za VVU na UKIMWI.

 

Tanzania ni miongoni mwa nchi maskini duniani yenye Pato Ghafi la Taifa kwa kila mtu kwa mwaka la Dola za Marekani 660. Tanzania ni ya 162 kati ya nchi 177 katika Faharasa ya Maendeleo ya Watu ya UNDP (2004). Umaskini umeenea nchi nzima. Tanzania imeanzisha mpango kabambe wa kupunguza umaskini unaojulikana kama MKUKUTA. Una shabaha ya kupunguza umaskini kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2010. Kwa mujibu wa makadirio ya mwaka 2000/2001 asilimia 36 ya watu wanaendelea kuishi chini ya Kiwango cha Umaskini wa Mahitaji ya Misingi, imepungua asilimia tatu tu ikilinganishwa na miaka 10 iliyotangulia. Kutokana na ongezeko la watu, idadi kubwa ya watu maskini imeongezeka katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Ingawa kiwango cha jumla cha kukua kiuchumi ni kati ya asilimia 5.7 na asilimia 6.7 kuanzia mwaka 2001 hadi 2004, kiwango cha kukua katika sekta ya kilimo kimekuwa cha chini kuliko sehemu nyingine za uchumi. Wakati umaskini unaweza kupungua sana Dar es Salaam, maeneo ya vijijini bila ya shaka huenda yakakosa kufikia shabaha iliyowekwa na MKUKUTA. Hakuna mlingano wa maendeleo nchi nzima na hii ni kwa mujibu wa viashirio mbalimbali. Wilaya chache zina chini ya asilimia 15 ya kaya chini ya kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi, hali ya kuwa katika wilaya nyingine asilimia inaweza kufikia 60. Hata hivyo baadhi ya wilaya maskini kabisa zimefanikiwa katika kupunguza kiwango cha vifo vya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano au kiwango halisi cha uandikishaji elimu ya msingi.

 

Kwa kawaida maendeleo ya uchumi hayakufikia hadi katika maeneo ya vijijini. Hata hivyo kuna miradi mingi kabambe ya sekta za miundombinu, mawasiliano ya simu, madini na utalii nchini na katika eneo lote la Afrika Mashariki, inayoweza kutoa fursa mpya kwa ajira na mapato katika sekta rasmi na isiyo rasmi. Hata hivyo inaweza kuingiza changamoto mpya kwa sababu kusafiri kutaweza kuongezeka na nyendo za wanaume peke yao nje ya familia zao na jamii kwa kufuata ajira (ya muda). Fursa hizo zinaweza kuweka mazingira ya kuenea kwa haraka kwa VVU na UKIMWI.