|
Mapitio ya Sera ya Taifa ya UKIMWI iliyopitishwa Mwaka 2001 |
|
|
TANGAZO: MAPITIO YA SERA YA TAIFA YA UKIMWI ILIYOPITISHWA MWAKA 2001
1.0 UTANGULIZI Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI – TACAIDS inapenda kuutangazia Umma kuwa imeanza mchakato wa kupitia Sera ya Taifa ya UKIMWI iliyopitishwa mwaka 2001. Mapitio hayo yameanza tangu tarehe 1 Novemba 2009. Ni matarajio ya Serikali kuwa zoezi lote litakuwa limekamilika katikati ya mwezi Machi 2010.
Chimbuko la mapitio haya ni mabadiliko na maendeleo mbalimbali ya kisayansi, kiteknolojia, kiuchumi na kijamii ambayo yametokea tangu mwaka 2001 Sera ya sasa ya UKIMWI ilipopitishwa. Aidha kumekuwa na changamoto nyingi ambazo zinatakiwa kuzingatiwa katika juhudi za kudhibiti UKIMWI nchini. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imechukua hatua mbalimbali za kudhibiti UKIMWI.
Hatua hizo zimejumuisha utoaji wa elimu kuhusu UKIMWI, huduma za matibabu zikijumuisha utoaji wa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI na huduma za matunzo. Vile vile tafiti mbalimbali zimeendelea kuendeshwa zikiwemo za chanjo ya UKIMWI. Serikali pia imetoa miongozo na mikakati mbalimbali tangu kipindi hicho ambayo inapaswa izingatiwe katika Sera.
2.0 USHIRIKI WA WADAU Serikali inapenda kuona wadau wanashiriki katika mchakato huu wa mapitio ya sera kwa kutoa maoni na mapendekezo yao. Hivyo Serikali inawaomba watu binafsi, Taasisi za Serikali, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia zikijumuisha Mashirika ya Dini, Vikundi vya Watu wanaoishi na UKIMWI pamoja na wadau wengine wa ndani na nje wajitokeze kutoa maoni yao. Maoni na mapendekezo yaelekezwe katika maeneo yaliyoainishwa hapa chini na mengineyo ambayo yataonekana ni muhimu na yanafaa kufikiriwa katika zoezi hili.
Masuala yapi ya sera iliyopitishwa mwaka 2001 ambayo bado ni muhimu yanafaa na hivyo yaendelee kuzingatiwa katika sera ijayo.
Ni masuala gani katika sera iliyopitishwa 2001 yamepitwa na wakati na hivyo hayastahili kujumuishwa katika sera ijayo.
Ni masuala yapi katika sera ya 2001 yanayohitaji kupitiwa upya ili yaendane na hali ya sasa au ya baadaye. Tafadhali toa mapendekezo unavyoona inafaa yarekebishwe.
Ni masuala gani mapya ambayo yanafaa kujumuishwa katika Sera mpya.
Maoni na mapendekezo yatumwe au kuwasilishwa kwa Mwenyekiti Mtendaji wa TUME YA KUDHIBITI UKIMWI – TACAIDS. Unaweza kuwasilisha maoni yako kwa kutumia tovuti ya TUME YA KUDHIBITI UKIMWI yenye anuani ifuatayo: www.tacaids.go.tz Unaweza pia kutuma maoni yako kwa maandishi kwa anuani ifuatayo (barua zote ziandikwe “Maoni ya mapitio ya será ya Taifa ya UKIMWI 2001”:-
MWENYEKITI MTENDAJI TUME YA KUDHIBITI UKIMWI S. L. P. 76987 DAR ES SALAAM
Barua Pepe:
This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it
Mwisho wa kupokea maoni ni tarehe 15 Desemba 2009.
|