News
TACAIDS YAPONGEZWA KWA KUTEKELEZA MALENGO YA KUPAMBANA NA UKIMWI
Kamisheni ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imepongeza Menejimenti ya Tume hiyokwa kujiwekea malengo yanayotekelezeka yenye lengo la kumaliza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza Julai 22,2024 jijini Dar es Salaam katika Kikao cha 57 cha Kamisheni, Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo, Dk. Hedwiga Swai, alieleza kuridhishwa na utendaji wa TACAIDS tangu alipochukua wadhifa huo.
Amesema katika kipindi hiki ambacho amekuwa Mwenyekiti, Dk. Swai amejifunza mengi na kuona jinsi TACAIDS inavyofanya kazi kwa ufanisi na ushirikiano mkubwa.
"Katika awamuzote mbili ambazo nimekuwa mwenyekiti wa tume hii, nimejifunza mengi na kugundua kuwa TACAIDS inafanya kazi kubwa kwa ushirikiano. Tulipotembelea miradi yenu, tuliona jinsi ambavyo mmefanikisha kwa kuwezesha vijana kujitegemea kupitia mradi wa Timiza Malengo," alisema Dk. Swai.
Dk. Swai aliongeza kuwa mradi wa Timiza Malengo umesaidia kupunguza maambukizi ya VVU miongoni mwa vijana kwa kuwawezesha kujitegemea kiuchumi, hivyo kupunguza vishawishi vya maambukizi.
Aidha, Dk. Swai amesisitiza umuhimu wa kueneza miradi kama hiyo (Timiza Malengo na Dreams) katika mikoa mingine kwa kutumia elimu na shughuli za ujasiriamali.
Kamisheni pia imepitishwa katika muundo mpya wa TACAIDS, ambao umezingatia mabadiliko muhimu kama vile kutenganisha nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni na Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS ili kuimarisha utawala bora na kuondoa nafasi ya Makamu wa Mwenyekiti Mtendaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TACAIDS, CPA(T) Yasin Abas, alieleza kuwa mabadiliko hayo pia yanajumuisha kuingiza Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI(ATF) ili kukabiliana na changamoto ya kukosekana kwa chanzo endelevu cha fedha, pamoja na kuondoa mwingiliano wa majukumu katika idara na vitengo ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
“Pia, TACAIDS imeanzisha Ofisi za Kanda ili kuimarisha uratibu wa mikoa na halmashauri, kugatua madaraka, na kushughulikia changamoto za kupata waratibu wa mikoa yote,” amesema Abas.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Jerome Kamwela, aliishukuru Kamisheni kwa uongozi thabiti na maelekezo yao, ambayo yameleta matokeo chanya kwa tume.
"Napenda kumshukuru Mwenyekiti na wajumbe wa Kamisheni kwa kuwa walimu wetu na viongozi thabiti. Maelekezo yenu yamekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya TACAIDS.
“Kwa ujumla, TACAIDS imeonesha dhamira thabiti katika mapambano dhidi ya UKIMWI na kujiwekea malengo yanayotekelezeka, ikilenga kumaliza UKIMWI ifikapo mwaka 2030, " alisema Dk. Kamwela.