News
BODI YA MFUKO WA UDHAMINI WA KUDHIBITI UKIMWI (ATF) YAKUTANA KUAJILI MAENDELEO YA MFUKO
Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (AIDS Trust Fund - ATF) imekutana jijini Dodoma kujadili maendeleo ya mfuko huo na kuweka mikakati ya kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake katika kusaidia jitihada za taifa za kudhibiti maambukizi ya UKIMWI.
Kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Sabasaba Moshingi, kimejikita katika tathmini ya utekelezaji wa shughuli za mfuko huo pamoja na kuhakikisha unaendelea kuwa chombo muhimu cha kufadhili afua mbalimbali za mapambano dhidi ya UKIMWI nchini.
Bodi hiyo imepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika mapambano dhidi ya UKIMWI kwa lengo la kulinda afya za wananchi na kufikia malengo ya kutokomeza tatizo hilo ifikapo mwaka 2030.
Aidha, Bodi imeitaka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ili kuhakikisha fedha zinazotolewa kupitia Mfuko wa ATF zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya UKIMWI nchini.
Vilevile, wajumbe wa Bodi wameeleza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi ili kuongeza rasilimali zitakazowezesha utekelezaji wa afua za kudhibiti UKIMWI na kuboresha maisha ya wananchi.

