News
KONGA YA WAVIU ILALA YATEMBELEA NA KUUZA BIDHAA ZAO BUNGENI
Dodoma
Konga ya Watu wanaoishi na VVU (WAVIU) -NACOPHA iliyopo wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam imepata fursa ya kutembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma na Kuuza Bidhaa wanazozalisha kwenye vikundi vya Konga hiyo.
Akieleza katika viwanja vya Bunge, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na VVU (NACOPHA) Mch. Emmanuel Msinga amesema wamefurahi kupata fursa ya kujionea jinsi shughuli za Bunge zinavyoendeshwa , kupata fursa ya kuuza bidhaa zao ndani ya viwanja vya Bunge pamoja na kukutana na Wabunge mbalimbali.
Aidha,ametoa shukrani kwa Spika wa Bunge na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Masuala ya Afya na UKIMWI kwa kuwapa mwaliko huo pia kukubali konga ya WAVIU Ilala iweze kutembelea na kuuza bidhaa zao ndani ya viwanja vya Bunge.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania Dkt. Adam Mrisho amesema TACAIDS itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu) na kuhakikisha afua za VVU na UKIMWI zinazowalenga WAVIU zinatekelezwa na kuleta matokeo Chanya katika kuchangia mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

