News
TACAIDS na Wizara za Kisekta Waja na Mpango Mkakati wa Vijana Kupunguza Maambukizi Mapya ya VVU
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa kushirikiana na wizara za kisekta ikiwemo Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii pamoja na waratibu wa masuala ya vijana katika Halmashauri na Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Kagera, Mbeya, Songwe na Iringa wamekutana kujadili namna ya kuandaa mpango mkakati endelevu wa programu za vijana.
Majadiliano haya yamelenga kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapata mazingira salama na rafiki, yanayowawezesha kuepuka hatari zinazoweza kuongeza uwezekano wa maambukizi mapya ya VVU. Hatua hii ni sehemu ya jitihada za kitaifa za kupunguza maambukizi mapya na kuimarisha afya ya jamii kwa vizazi vijavyo, majadiliano hayo yamefanyika leo Februari 4, 2025 jijini Dodoma.
TACAIDS na wizara husika wamesisitiza kuwa vijana ndio nguzo ya taifa na wanapaswa kupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kupanga na kutekeleza programu zinazohusu maisha yao. Kupitia mpango huu, serikali inalenga kuimarisha elimu ya afya, kuongeza upatikanaji wa huduma rafiki kwa vijana, na kuendeleza kampeni za uhamasishaji zinazojikita katika kujenga tabia salama.
Kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na jamii, mpango huu unatarajiwa kuwa chachu ya kupunguza maambukizi mapya ya VVU na kuimarisha ustawi wa vijana, huku ukitoa dira ya taifa katika mwitikio wa UKIMWI wa muda mrefu.

