News
KAMPENI YA KILI CHALLENGE 2025 YAZINDULIWA RASMI NA SERIKALI
Dar es Salaam, Tanzania – Aprili 25, 2025
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), leo imezindua rasmi kampeni ya Kili Challenge 2025, yenye lengo la kuchangisha fedha za ndani kusaidia mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.
Mgeni rasmi, Mhe. Jerry Slaa, akimuwakilisha Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Doto Biteko, aliwaongoza wadau mbalimbali kutoka Serikalini, sekta binafsi, na taasisi za kiraia kushuhudia tukio hilo muhimu lililofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake, Mhe. Jerry Slaa alisisitiza kuwa “Kili Challenge si tukio la kawaida, bali ni jukwaa la mshikamano kati ya Serikali, sekta binafsi na wananchi katika kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.”
Aidha, alitumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri na kwa kuweka kipaumbele katika ajenda ya kutokomeza UKIMWI nchini. Alisema kuwa juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita zimeonesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha kila Mtanzania anaishi maisha yenye afya na ustawi.
TACAIDS kwa kushirikiana na Kampuni ya Geita Gold Mine (GGML) na AngloGold Ashanti, imekuwa ikiendesha kampeni hii kwa miaka 23 sasa. Kupitia Mfuko wa Kili Trust, mamilioni ya Watanzania wamepata huduma za kinga, tiba na matunzo ya VVU, hususan katika maeneo ya wachimbaji wadogo, wavuvi, na makundi yaliyo hatarini zaidi.
Serikali imetoa wito kwa makampuni, taasisi, na mashirika yote nchini kushiriki kikamilifu kwa kuchangia fedha, kushiriki katika shughuli za kampeni kama kupanda Mlima Kilimanjaro au kuzunguka kwa baiskeli, na kushirikiana na TACAIDS kuweka mikakati ya muda mrefu ya uendelevu wa afua za VVU na UKIMWI.
“Huu si wakati wa kutazama pembeni. Ni wakati wa kila mmoja wetu kuwa sehemu ya historia ya kizazi kisicho na maambukizi mapya ya VVU,” alisisitiza Mhe. Jerry Slaa.