Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania
The Prime Minister's Office

Tanzania Commission for AIDS

Tanzania Commission for AIDS

News

​TACAIDS, WIZARA YA AFYA NA OR-TAMISEMI WAJADILI NAMNA YA KUIMARISHA URATIBU WA UKIMWI WA KISEKTA NCHINI


Dodoma, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imeratibu mkutano uliolenga kuimarisha uratibu wa afua za UKIMWI wa kisekta pamoja na kuimarisha uhimilivu wa utekelezaji wa shughuli za VVU na UKIMWI nchini. Mkutano huo uliofanyika leo tarehe 27 Machi 2025, umehudhuriwa na washiriki kutoka TACAIDS, Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa (OR – TAMISEMI). Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Catherine Joachim amesema jukumu kubwa la TACAIDS ni kusimamia uratibu wa UKIMWI wa kisekta ili kuhakikisha malengo ya Serikali ya kutokomeza UKIMWI ifikapo 2030 yanafikiwa. "TACAIDS tumeona tuitishe mkutano huu tuweze kujadiliana namna tutakavyoweza kuboresha uratibu wa mwitikio wa UKIMWI wa kisekta kwenye ngazi zote ili kuleta tija na ufanisi kulingana na rasilimali tulizonazo na kuleta matokeo chanya” amesema Dkt. Catherine. Akizungumza kwa niaba ya OR-TAMISEMI Dkt. Mwanahamisi Hassan amesema OR – TAMISEMI iko tayari kushirikiana na Wizara na taasisi nyingine ili kuimarisha utekelezaji wa shughuli za VVU na UKIMWI kwenye ngazi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa na kuhakikisha Serikali inafikia malengo yaliyowekwa katika kutokomeza UKIMWI. Naye Mkuu wa Programu za UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria kutoka Wizara ya Afya Dkt. Samwel Lazaro amesema Wizara inatambua umuhimu wa kushirikiana ili kutokomeza UKIMWI nchini hivyo iko tayari kujadili na kuboresha uratibu wa kisekta katika utekelezaji wa mwitikio wa UKIMWI ikiwa ni pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma za UKIMWI kwa mujibu wa sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa na Serikali. Miongoni mwa mambo muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na hali ya VVU na UKIMWI nchini, hatua zilizofikiwa katika kuimarisha uhimilivu wa utekelezaji wa shughuliza UKIMWI, hali ya upatikanaji wa rasilimali za ndani za UKIMWI kupitia mfuko wa UKIMWI (ATF), uratibu wa shughuli za UKIMWI ngazi ya Kanda, Mikoa na Halmashauri, mifumo ya taarifa za VVU na UKIMWI pamoja na utoaji wa huduma za UKIMWI kupitia vituo vya maarifa **MWISHO**