Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania
The Prime Minister's Office

Tanzania Commission for AIDS

Tanzania Commission for AIDS

News

TACAIDS YAENDESHA MAFUNZO KWA KAMATI MPYA YA UKAGUZI ILI KUIMARISHA USIMAMIZI NA UTAWALA BORA


Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imeanza mafunzo maalum kwa Kamati yake mpya ya Ukaguzi, ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha usimamizi, uwajibikaji na utawala bora ndani ya taasisi hiyo.

Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi leo Septemba 17, 2025 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt. Samwel Sumba, ambaye amesisitiza umuhimu wa uelewa wa majukumu ya Kamati ya Ukaguzi na ushirikiano wa karibu kati ya kamati hiyo na menejimenti ya taasisi.

“Tunatambua kuwa mafanikio ya taasisi yoyote yanategemea uwazi na uwajibikaji. Mafunzo haya ni jukwaa la kujenga uelewa wa pamoja na kuimarisha misingi ya utawala bora,”

Aidha, Dkt. Sumba amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kusaidia Kamati ya Ukaguzi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, hususan katika kuhakikisha uadilifu na uwazi vinadumu katika kila ngazi ya utendaji wa TACAIDS.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya TACAIDS, David Alal ameishukuru menejimenti ya tume kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa yamewasaidia kuelewa kwa kina namna taasisi inavyofanya kazi zake.

“Mafunzo haya yametupa mwanga mpana kuhusu majukumu yetu na jinsi ya kushirikiana na menejimenti kwa ufanisi zaidi,”

Miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika mafunzo hayo ni pamoja na Sheria ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, muundo na majukumu ya tume, Mkakati wa Tano wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (2021/22 - 2025/26), pamoja na Mpango Mkakati wa TACAIDS wa miaka mitano (2021/22 - 2025/25).

Hatua hii inaonesha dhamira ya TACAIDS kuendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi na kuhakikisha kuwa taasisi inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.