Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania
The Prime Minister's Office

Tanzania Commission for AIDS

Tanzania Commission for AIDS

News

​UZINDUZI WA KAMPENI YA KILI CHALLENGE 2025: TACAIDS YATOA WITO WA KUUNGA MKONO JITIHADA ZA KUTOKOMEZA UKIMWI


Dar es Salaam. Tarehe 25 Aprili, 2025

Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), kwa kushirikiana na kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), imezindua rasmi kampeni ya Kili Challenge 2025, harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI kupitia Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI (AIDS Trust Fund – ATF).

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt. Catherine Joachim, alieleza kuwa kampeni ya Kili Challenge ni mfano bora wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kuchangia afya ya jamii, hususan kwa makundi yaliyo hatarini kama vijana, WAVIU, wachimbaji wadogo, watoto yatima, na wengineo.

“Kupitia kampeni hii, tumeweza kuongeza uhamasishaji, kuboresha upatikanaji wa huduma, na kutoa matumaini kwa maelfu ya Watanzania. TACAIDS itaendelea kuwashirikisha wadau wa sekta binafsi, taasisi za kifedha, makampuni ya simu, migodi, na jamii kwa ujumla ili kuongeza mchango kwenye Mfuko wa ATF,” alisema Dkt. Catherine.

Kwa sasa, Tanzania imepiga hatua katika kufikia malengo ya kimataifa ya 95-95-95, ikiwa imefikia 82.7% ya watu wanaojua hali zao za VVU, 98% walioko kwenye matibabu, na 94% waliofubaza virusi. Hata hivyo, bado kuna haja ya kuwekeza zaidi ili kufikia asilimia 95 kwa kila kipengele ifikapo 2030.

Uzinduzi huu ni mwanzo wa safari ya Kili Challenge 2025, ambapo tarehe 18 Julai 2025 washiriki wataanza kupanda Mlima Kilimanjaro, na tarehe 24 Julai 2025 watafikia kilele cha harambee hiyo ya kihistoria.

TACAIDS inatoa wito kwa kila Mtanzania, taasisi na makampuni kushiriki kikamilifu katika kampeni hii na kuonyesha uzalendo wao kwa kuchangia ustawi wa Taifa letu kupitia Mfuko wa ATF.