News
WATUMISHI WA TACAIDS WAPATIWA MAFUNZO YA MAADILI NA MABADILIKO YA USIMAMIZI
Watumishi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) wanapatiwa mafunzo kuhusu Maadili na Mabadiliko ya Usimamizi ili kuboresha utendaji kazi na kufikia malengo ya taasisi. kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma. Aidha, mafunzo haya yanalenga kuimarisha ushirikiano kati ya watumishi katika uratibu wa mwitikio wa UKIMWI hapa nchini.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt. Catherine Joachim alisema, Menejimenti ya TACAIDS imeona kuna umuhimu kwa watumishi kupatiwa mafunzo hayo kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aliwasisitiza watumishi kutumia fursa ya mafunzo haya kama chachu ili kufikia malengo ya kimkakati ya kutokomeza UKIMWI ifikapo 2030.
“Utendaji wetu wa kazi unahitaji kubadilika ili kukabiliana na mabadiliko mbalimbali yanayoendelea”. Alisisitiza Dkt. Catherine.
Kwa upande wa mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma, tawi la Singida Bw Jesse Mashimi, aliwasisitiza watumishi kuwajibika na kutekeleza majukumu yao kama timu.
“Kufanya kazi kama timu ndio njia pekee ya kufikia malengo ya taasisi pamoja na kuzingatia kwamba kila mmoja ana muhitaji mwenzake ili majukumu na malengo yaweze kufikiwa” alisisitiza Prof. Machimi.